NA SHAIB KIFAYA
Wafanyakazi wa tasisi za serikali wametakiwa kuwa na utaratibu wa kuchunguza afya zao ili kujilinda na maradhi.
Hayo yalilezwa na Ofsa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba, Shadya Shaban Seif, wakati akizindua zoezi la uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa taasisi za serikali lililofanyika Gombani Chake Chake Pemba.
Alisema imeonekana kwamba wafanyakazi wengi hawana muda wa kufika hospitali kuchunguza afya zao ndio maana wizara kwa kushirikiana na madaktari kutoka China wakaamua kuandaa mpango wa kuwafuata sehemu zao za kazi kupima afya zao.
Aliwahimiza wafanyakazi hao, kufanya mazoezi mara kwa mara na kupunguza kula vyakula vya mafuta, ili kuepuka ugonjwa wa shindikizo la damu (presha) ambao unawapata watu wengi.
“Kuleni zaidi vyakula vya matunda kwa kuimarisha afya zanu, epukeni kula vyakula vya mafuta, kwani hivyo sio vizuri kwa afya,” alisema.
Kiongozi wa timu ya madaktari kutoka China wanaofanya kazi katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, Dk. Yuan Tongzhou alisema, lengo la zoezi hilo ni kuwasaidia wafanyakazi hao kupata muda mzuri wa kuwatumikia wananchi wakiwa hawana wasi wasi kuhusu maradhi.
“Tangu tulipofika katika hospitali hii ya Mkoani tumekuwa na utaratibu wa kuwafuata wananchi vijijini kuwachunguza afya zao, lakini leo hii tumewafuata wafanyakazi, kwani na wao hawana muda wa kuifuata huduma hii hospitali au vituo vya afya, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao,” alisema.
Alisema kutokana na uhusiano mzuri walionao kati yao na serikali, wamefanya hivyo kwani ni miongoni mwa kuendeleza urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya China na Zanzibar. Ofisa Mdhamini Wizara ya Katiba na Sheria Pemba, Mattar Zahor, aliupongeza uongozi wa wizara ya afya kwa kuwapatia huduma hiyo.