NA HAFSA GOLO

HALMASHAURI ya Kaskazini “A” Unguja imewataka wafugaji kuondokana na utamaduni wa kuwachia mifugo yao ama kuyafunga katika mashamba ya watu kwani sio desturi wala utamaduni mzuri.

Msaidizi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ngwali Makame Haji, alieleza hayo wakati akizungumza na gazeti hili katika  muendelezo wa ziara maalumu ya kusikiliza kero za wakulima iliyofanyika Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.

Alisema ni vyema wafugaji  na watu wengine kudumisha utamaduni wa kuheshimiana na kuthamini juhudi za wakulima hasa ikizingatiwa wanatumia gharama na nguvu kubwa katika kustawisha kilimo chao.

Aidha alisema iwapo itabainika mtu yoyote kufunga mnyama wake katika shamba la mkulima hatua kali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kulipa gharama yote iliyosababishwa na mnyama aliemfunga katika shamba la mkulima.

Alisema katika kuhakikisha changamoto na malalamiko  ya wakulima juu ya uharibifu wa mazao yao yanayotokana na ufungwaji wa wanyama katika mashamba yao unadhibitiwa wataendelea na utoaji wa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa kufuata taratibu sambamba na athari za ukiukwaji wa miongozo ya kisheria . 

Mapema mmoja ya wakulima Patima Vuai Mwita alisema kwamba anasikitishwa na tabia inayofanywa na baadhi ya watu wanaofuga ngombe na mbuzi katika maeneo ya kilimo na hatimae kuharibu mazao yao.

“Changamoto ya ufugaji wa Ng’ombe na Mbuzi katika maeneo ya kilimo bado ni tatizo linalotusumbua tunaomba tusaidiwe katika kulikomesha”,alisema

Nae Khadija Kombo alisema,kitendo cha wafugaji kuwaachia watoto kwenda kuwalishia wanyama wao nacho kinachangia kuimarika kwa vitendo vya uharibifu wa mazao katika maeneo ya kilimo.