KINSHASA,CONGO
WAFUNGWA 52 wa jela moja ya mji wa Bunia kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefariki dunia kutokana na njaa mwaka huu wa 2020.
Wafungwa hao walifariki kwa kukosa chakula baada ya Serikali ya nchi hiyo kushindwa kutoa fedha za kutosha.
Jela za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni miongoni mwa jela zenye msongamano wa wafungwa wengi duniani na wafungwa wanasumbuliwa na mgao duni wa chakula.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, jela hiyo ya Bunia inafanya kazi zaidi ya uwezo wake wa kawaida kwa asilimia 500.
Ferdinand Fimbo Meya wa mji wa Bunia alisema kuwa, hali hiyo inatisha sana na aliilaumu Serikali ya Kinshasa kwa kusababisha utapiamlo katika jela hiyo.
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi huu aliliambia baraza lake la mawaziri kwamba, atahakikisha kuwa jela zote nchini humo hazipungukiwa na chakula wala madawa.
Hata hivyo mkuu wa jela ya Bunia,Camille Zonzi alinukuliwa katika ripoti ya kikosi cha kulinda amani huko Congo akisema kuwa, Serikali iliahidi katika mkutano wa wiki iliyopita kwamba itatoa fedha za matumizi ya miezi mitatu kwa ajili ya jela hiyo.
Shirika la Human Rights Watch linasema kuwa utapiamlo limekuwa jambo la kawaida katika jela za Congo kutokana na chakula kutogawiwa kwa mujibu wa idadi ya wafungwa.