NA MARYAM SALUM, PEMBA
WAGOMBEA nafasi mbali mbali za uongozi, ikiwemo nafasi ya Ubunge Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamesema endapo watapata ridhaa za kuchaguliwa na wananchi kuongoza majimbo husika, watahakikisha wanalinda mafanikio ya maendeleo yaliyopo.
Waliyasema hayo katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika katika kiwanja cha Gando, wakati wakitambulishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambae pia ni Rais wa Zanzibar, Dk,
Ali Mohamed Shein, katika eneo hilo.
Wagombea hao, walisema kuwa endapo wananchi, wanachama wa Chama cha Mapinduzi pamoja na wapenda maendeleo ya nchi watawachagua wagombea hao, basi watahakikisha wanalinda na kuendeleza maendeleo zaidi kwa maslahi ya jamii.
“Sisi hatutotoa ahadi kwamba wananchi tutawapatia ajira moja kwa moja kutoka Serikali kwa vile hatuna uwezo huo kutokana na nafasi zetu, bali tutahakikisha tupo na mashirikiano zaidi na Serikali katika kuendeleza maendeleo ndani ya jamii,” walisema.
Walisema kuwa kama Wabunge, Wawakilishi, Madiwani na viti maalum,wa mkoa huo endapo watapata ridhaa za wananchi kuongoza, wataendeleza umoja na mashirikiano katika kusaidiana kwenye suala la maendeleo.
“Kutokana na nafasi zetu ambazo tunagombea, hatutokuwa na uwezo wa kuwapa ahadi kwamba tutawapatia ajira, bali tutasaidiana katika kuboresha wajasiriamali wa vikundi vya maendeleo, na kuwapatia nyenzo nyengine zitakazowainua kiuchumi,” walisema wagombea hao.
Mgombea Uwakilishi jimbo la Gando, Maryam Thani Juma, alisema kuwa jimbo hilo limekuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwa muda wa miaka minne toka kushika nafasi hiyo.“Jimbo la Gando limekuwa na mabadiliko ya kimaendeleo, tukilinganisha na hapo kabla yake, hivyo wananchi msikubali kuburuzwa angalieni mafanikio mliyoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi kutoka kwa viongozi wake wanaongoza,” alisema.