NA TATU MAKAME

MGOMBEA wa nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja, Asha Abdalla Mussa, amesema endapo atachaguliwa kuliongoza jimbo hilo atahakikisha anatekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa vitendo ili kuleta mabadiliko.

Asha alisema hayo Uwanja wa mpira Kilombero Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja wakati akiomba kura kwa wananchi wa Jimbo hilo mara baada ya uzinduzi wa kampeni wa jimbo hilo.

Alieleza kuwa utekelezaji wa ilani ndio njia pekee itakayoleta heshima na Imani kwa wananchi, hivyo atahakikisha anafanyakazi ya kuwatumikia wananchi na kuleta mabadiliko.

Alisema katika utekelezaji huo atahakikisha maeneo yote yaliyoainishwa katika ilani anayatimiza kwa kushirikiana na viongozi wengine ikiwemo huduma za jamii, afya elimu, maji, safi na salama ,barabara za ndani na huduma nyengine hivyo aliwataka wananchi kuwachagua.

Nae Mgombea wa nafasi ya Ubunge katika Jimbo hilo Abdalla Ali Hassan Mwinyi, alisema katika kutekeleza Ilani wananchi wategemee neema katika uongozi wake na aliwahakikishia kuwa ataondosha mifarakano na mivutano ya kisiasa katika uongozi wake na kuahidi kuleta mabadiliko.