NA ASYA HASSAN

WANANCHI nchini wamesisitizwa kuendelea kudumisha amani na utulivu iliyopo nchini, ili iweze kuchochea kasi ya maendeleo ya jamii.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Magharibi ‘A’, Dk. Said Haji Mrisho, alipokuwa akizungumza na Zanzibarleo hili na kueleza kuwa amani na utulivu vina mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii hivyo ipo haja ya kuenziwa.

Alifahamisha kwamba Zanzibar, imepiga hatua kubwa za maendeleo katika nyanja mbalimbali kutokana na uwepo wa hali hiyo, jambo ambalo lisingewezekana kama ingekuwa kinyume chake.

Alisema ni muhimu kwa kila mwananchi kuiunga mkono serikali kwa kuhubiri na kuitunza amani iliyopo, ili izidi kudumu kwani ndio silaha ya maendeleo duniani.

“Amani ya nchi hujengwa au huvunjwa na wananchi wenyewe, hivyo ni vyema kila mwananchi akajiepusha kufanya mambo yanayoashiria uvunjifu wa amani kwani yeyote atakaebainika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alieleza Dk. Mrisho.