NA MARYAM HASSAN

WAKULIMA nchini wametakiwa kuitunza miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza tija katika kilimo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa idara ya umwagiliaji maji, Haji Hamid alipokuwa akizungumza na viongozi wa mabonde mapya yaliyowekewa miundombinu ya umwagiliaji maji.

Aliwaomba viongozi hao kuhakikisha wanafuata maelekezo wanayopatiwa juu ya namna bora ya utunzaji wa miundombinu hiyo itumike kwa muda mrefu.

“Kutokana na miundombinu hii, mkawasimamie wakulima wenu kupanga kalenda ya kilimo na ratiba nzuri ya umwagiliaji ili kuepusha migogoro,” alisema Haji.

Sambamba na hayo pia aliwataka kuwa na mwamko wa kuchangia pindi itapotokea miundombinu hiyo imeharibika na inahitaji kutengenezwa.  

Akizungumza baada ya ziara katika baadhi ya maeneo, mtaalamu wa kilimo wa Idara ya umwagiliaji na miundombinu ya kilimo kutoka mkoa wa Morogoro Heaven Jesse, alisema endapo miundombinu hiyo itaendelezwa, uzalishaji wa mpunga utaongezeka na kuwakomboa wananchi na umasikini wa chakula.

“Serikali inathamini jitihada zinazochukuliwa na wakulima kwa sababu ndio muhimili mkuu wa uchumi ndio maana inachukua hatua za kuwawezesha katika kila hatua,” alisema mtaalamu huyo.

Ziara ya wakuu hao wa idara hizo inayohusisha viongozi wa mabonde yote ya umwagiliaji wa Unguja na Pemba ina lengo la kutoa mafunzo kwa viongozi hao ili waendeleze kilimo cha mpunga katika kipindi chote cha mwaka.