NA AMEIR KHALID

WANAFUNZI waliomaliza shahada ya kwanza ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka katika Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), wametakiwa kuthamini elimu hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa katika ofisi zao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Idara za Miundo ya Taasisi, Utumishi na Maslahi ya Watumishi, kutoka Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Shaib Ally Mwazema, wakati akizungumza na wanafunzi hao kwenye hafla maalum ya kupongezana baada ya kumaliza masomo yao huko Chuo cha IPA Tunguu.

Alisema masjala ni sehemu muhimu sana na nyeti ambayo serikali na taasisi nyingine inaithamini hivyo na wao vyema wakatambua umuhimu wake katika kutelekeza majukumu yao.

“Masjala ikiwa mbovu, ofisi haiwezi kufanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa, hivyo nawaombeni kuwa makini sana na kutambua umuhimu wa kazi yenu ambayo,’’ alisema.

Aliongeza kuwa tabia ya baadhi ya watumishi wa masjala kupoteza majalada ya watumishi kunaweza kuwahatarisha usalama wao wa kazi, hivyo lazima kuwa makini na kazi yao hiyo.

Hivyo aliwataka wahitimu hao kuleta mabadiliko katika taasisi zao, kwani bila ya kufanya hivyo watakuwa hawaitendea haki elimu waliyoipata ambayo waliihangaikia kwa kipindi cha miaka mitatu.

Aidha aliwaomba kuendelea kusoma zaidi na wasitosheke pale walipofika, huku serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiendelea kuajiri watu wenye sifa katika sehemu husika.

Mapema Mrajisi wa chuo hicho Mshauri Abdulla Khamis aliwanasihi wahitimu hao kuzingatia fani yao ili kuwavutia na watu wengine kujitokeza kwenda kusoma.

Aliwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri kwa kukitangaza chuo, kwa kufanya kazi kwa bidiii na kufuata sheria za utumishi ili kujiepusha na matatizo yasiyo ya lazima.

Katika risala yao wanafunzi hao wameuomba uongozi wa chuo kutatua baadhi ya changamoto zinazovikabili vyuo ikiwemo vifaa vya kufundishia wakati wa mazoezi ya vitendo.

Jumla ya wanafunzi 27 wamemaliza masomo ya shahada ya kwanza ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka iliyotolewa na Chuo cha Utawala wa Umma (IPA).