NA MWAJUMA JUMA

WIZARA ya Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto imejipangia kutoa mikopo 700 kwa vikundi vya kiuchumi na wajasiriamali mmoja mmoja kupitia Mfuko wa Uwezeshaji.

Mikopo hiyo yenye thamani ya shilingi Milioni 850, inatarajiwa kutolewa kwa sekta zote za kiuchumi katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Waziri wa Wizara hiyo Mouldline Cyrus Castico aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa jukwaa la wanawake Milioni 50 wa kiafrika, uliofanyika ukumbi wa mamlaka ya udhibiti wa maji na nishati (ZURA) mjini Zanzibar.

Alisema kuwa takwimu za kiuchumi duniani zinaonesha kuwa sekta ya Ujasiriamali imeendelea kukuwa na hivyo kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ikiwemo kuzalisha ajira.

Hata hivyo alisema kuwa mwaka wa fedha 2019/2020 mfuko huo ulitowa mikopo 811 Unguja na Pemba yenye thamani ya shilingi milioni 789.35 kwa wajasiriamali mbali mbali.

Alisema kuwa kati ya mikopo hiyo iliyotolewa, mikopo ya vikundi ni 223, vikiwemo vikundi 42 vya makundi maalumu ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na vilivyobakia 181 ni vikundi mchanganyiko.

Castico alisema kuwa jumla ya wajasiriamali 5,092 walinufaika na mikopo hiyo, kati ya hao wanawake ni asilimia 53.

Sambamba na hayo alisema kuwa uzinduzi wa jukwaa hilo la wanawake umefanywa kwa lengo la kuwahamasisha wanawake kufanya biashara kwa njia ya kimtandao na kuweza kupanuwa zaidi na kuelekea kwenye mtandao wa Afrika Mashariki na kufikia mtandao wa kikanda na kimataifa.

Hivyo alitumia fursa hiyo kushukuru sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuratibu utekelezaji wa mradi huu, ambao ni muhimu kwa maendeleo ya wanawake na wajasiriamali hapa nchini.

Alifahamisha kwamba katika takwimu za dunia za mwaka 2014 zinaonesha asilimia 80 ya wazanzibari wapo katika sekta hiyo, ambapo asilimia 47 ya wajasiriamali wanawake wanajishughulisha na biashara.

Mapema Katibu wa masuala ya Kijamii kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki Christophe Bazisamo aliwataka wanawake wa Kizanzibari kuchamgamkia fursa hiyo ambayo ni maalumu kwao katika kujiendeleza kiuchumi.