NA HAFSA GOLO
WAKULIMA wa Shehia ya Mkwajuni wamepatiwa elimu ya kilimo cha mpunga ili kutekeleza majukumu yao kwa utaalamu na kuleta tija katika msimu wa kilimo wa 2020/2021.
Hayo yamebainika wakati timu ya wataalamu wa kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja ilipofanya ziara ya kuwatembelea wakulima wa shehia hiyo hivi karibuni.
Msaidizi Mkurugenzi wa huduma za jamii kilimo katika halamashauri hiy, Ngwali Makame Haji, alisema hatua hiyo itakuwa endelevu katika mabonde yote yanayolimwa mpunga ili kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la uzalishaji kukidhi mahitaji wa wakulima.
Alisema utaratibu huo utakuwa sambamba na usikilizaji wa kilio cha wakulima katika kukabiliana na kilimo hicho na kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi kwa wakati muafaka na kutimiza malengo ya serikali ya kupunguza uagiziaji wa mchele kutoka nje.
Ngwali alisema katika kufikia malengo ya serikali, atahakikisha wakulima wanafanya matayarisho mazuri na kuwapatia wakulima pembejeo ikiwa pamoja na mbegu bora.
Aidha alisema, mavuno msimu wa kilimo cha zao hilo mwaka uliomaliza yalikuwa mazuri ambapo katika eka wakulima walivuna wastani wa kilo 900 katika maeneo ambayo yalilimwa kwa kufuata miongozo, taratibu na kanuni za kilimo.
Akizungumzia kuhusu suala la wataalamu, alisema wilayani humo wapo wa kutosha wakiwemo mabibi na mabwana shamba ambao wamekuwa wakisimamia vyema majukumu yao.