NA MWANAJUMA MMANGA

MKURUGENZI  wa Bodi ya Huduma za Maktaba,  Sichana Haji Foum, amewataka walimu kuendelea kutumia mbinu bora za ufundishaji zitakazosaidia wanafunzi kujua kusoma na kuandika

Aliyasema  hayo katika maadhimisho ya siku ya kusoma na kuandika duniani huko skuli ya Kinuni na Mwenge ambapo alisema hatua hiyo itasaidia kufanikisha azma ya serikali ya kuendeleza sekta ya elimu nchini .

Alisema misingi bora ya mwanafunzi ni kujua kusoma na kuandika, ambapo kutamsaidia kukua kielimu na kufikia ndoto zao, hivyo ni vyema walimu kujitahidi juu ya hilo.

Alisema  lengo la siku hiyo ni kutathmini hali ya usomaji na uandikaji kwa wanafunzi pamoja na kuboresha huduma za maktaba katika skuli mbali mbali.

Aidha ameitaka jamii kuona umuhimu wa kuzitumia huduma za maktaba zilizo karibu nao, ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Alisema  serikali inaendelea na jitihada mbali mbali za kusogeza huduma muhimu maeneo ya karibu, ili kuwaondoshea usumbufu wananchi wake na amewataka wanafunzi kupenda kusoma  ili kuweza kuwasaidia katika kujibu mitihani ya moko na taifa kwa ujumla. 

Hata hivyo amewasisitiza  wanafunzi hao kuzitumia Maktaba kwa kujisomea ili kuwasaidia mambo mengi ya masomo yao wanayosoma.