NA HUSNA SHEHA

WAZAZI na walezi wametakia kushirikiana na walimu katika malezi hasa mazingira ya masomo ya watoto wao, pamoja na kuchukua jukumu la kuwafahamisha suala la udhalilishaji katika jamii.

Hayo yalielezwa na mwanaharakati anaeshughulikia mambo ya udhalilishaji katika Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, Asha Masoud Sanani, wakati akitoa elimu ya udhalilishaji kwa wazazi, walezi na wanafunzi wa skuli hiyo.

Alisema vitendo vingi vya udhalilishaji mara nyingi vinawapata wanafunzi hivyo ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha wakati wote wanashirikiana na walimu katika kuwalinda watoto wao hasa nyakati za kwenda skuli na kurudi.

Mwanaharakati huyo alibainisha kuwa wazazi wengi hawana muamko wa kufatilia maendeleo ya watoto wao maskulini, jambo ambalo linawavunja moyo walimu, ambapo watoto wengi wamekuwa wakiinga vitendo vya kingono hasa katika mitandao ya kijamii na kujiingiza na kubebeshwa ujauzito.

Alisema zipo kesi nyingi za udhalilishaji zinajitokeza katika shehia hiyo jambo ambalo limemuamsha ari ya kutafuta wataalamu kwa ajili ya kutoa elimu, ili kujikinga na vitendo hivyo.

 “Ikiwa wazazi, walezi na watoto, tutaondosha muhali wa kuwafichua wahalifu hawa basi kesi nyingi za udhalilishaji zinaweza kutolewa hukumu stahiki, lakini mkiendelea kuwaficha wahalifu kwa kuhofia uhasama hatutafika kwani hata Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein anachukia vitendo hivi, ” alisema

Sambamba na hayo aliwashauri wazazi kurudisha malezi ya zamani ili jamii iwe salama kimaadili na kuwapata viongozi madhubuti wa baadae watakaolitumikia taifa lao katika nyanya mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo.

Pia aliwataka wazazi kuwacha muhali kwa wahalifu kwa kurubuniwa kwa fedha ama kitu fulani pindi pale mtoto anapodhalilishwa ,ni vyema kumchukulia hatu zinazofaa kwa kuripoti kwa sheha wa shehia na kuchukuliwa hatua za kisheria

“Wazazi tusikubali kuhadaliwa na wahalifu kwa kupewa pesa ama kitu cha thamani, ili msitoe ushahidi au kesi msiripoti polisi na kumalizana wenyewe kwa wenyewe sio jambo zuri, hasa kwa mtoto aliyedhalilishwa,”alisema.

Nae Sheha wa Shehia hiyo, Subira Haji Yahya, aliwataka wanafunzi wataofanyiwa udhalilishaji wa aina yoyote ikiwa ya kingono ya mateso majumbani kutoa taarifa sehemu husika au kwa mtu aliyekuwa karibu nae, ili apate kuchukuliwa hatua za sheria.

Aidha aliwataka wasilipuuze suala hilo kwani linazidi kushamiri hasa katika sehemu ya skuli kama zinavyosikika katika vyombo vya habari mbali mbali.

Hata hivyo, aliahidi kuendelea kuotoa elimu mara kwa mara katika skuli hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wanajikinga na vitendo vya udhalilishaji.