NA HAFSA GOLO
VIJANA waliotoka chama cha upinzani cha CUF wamelaani kauli za uchochezi zinazoashiria uvunjifu wa amani nchi kuelekea uchaguzi mkuu zinazotolewa na baadhi ya vyama vya upinzani vilivyoingia katika uchaguzi unaotarajiwa Oktoba 28 mwaka huu.
Walieleza hayo wakati wakizungumza na vyombo mbali mbali vya habari katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kiwajuni, ambapo alisema kauli hizo zinastahiki kukemewa kwa nguvu zote kutokana zinaashiria kuleta uvunjifu wa amani iliopo nchi ambayo ndio wanayojivunia ambapo mataifa mengi duniani wanaitamani baada ya kuichezea.
Mmoja wa vijana hao ambae alikuwa Mbunge kupitia chama hicho jimbo la Chake Chake, Yussuf Kaiza Makame, aliwataka vijana kuepuka wanasiasa ambao wamekuwa ni sehemu ya kuchochea na kuhamasisha vurugu ambazo zitapelekea kuhatarisha amani ya nchi.
Aliongeza kwamba hakuna mbadala wa amani iwe ndani ya kijiji.mkoa hata taifa hivyo, ni vyema wananchi kulinda heshima na utu wao na sio kubaguana .
Akigusia suala la umasikini alisema sio chanzo cha wanachi kujikubalisha kuleta vurugu wala kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kwani hata nchi zilizoendelea umasikini upo.
Hivyo, alisema ni wakati kwa wananchi kutunza hazina ya amani iliyopo hasa ikizingatiwa miongoni mwa waathirika wakubwa ni wazee, wanawake na watoto.
Akigusia masuala ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni alisifu sera na ilani ya CCM ambazo zinasisitiza umuhimu wa amani mchini.