KWA muda sasa kwa kutumia nafasi yetu katika jamii kama chombo cha habari tumekuwa tukisisiza umuhimu amani kwasababu tunaamini rasilimali ya amani ndiyo injini ya kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu na wananchi kwa ujumla.

Muda huu tumekuwa tukisisitiza umuhimu wa amani kwa sababu uzoefu unaonesha kuwa kipindi kama hichi hasa cha kampeni kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, amani hupitia kwenye majaribu yasiyo ya kawaida.

Majaribu ya kutetereka kwa amani katika nchi kwenye kipindi kama hichi hutokana na mihemko inayotokana na hamasa za kisiasa za kupita mipaka ambapo wafusi wengi wa vyama husikiliza na kuziamini kauli za viongozi wao bila ya wakati mwengine kuzipima kauli hizo.

Kwa hiyo kiongozi wa kisiasa anapokusanya wafusi kwenye mkutano wake wa kampeni pasi na kuipima kauli yake anayotaka kuitoa kwa wafusi wake, kauli hizo zinaweza kutekelezwa kwa vitendo na wafuasi hao bila ya kujali kwamba wanavunja sheria.

Viongozi wa kisiasa katika wakati huu lazima watambue kwamba wapo baadhi ya wafusi wengi ambao hawana uwezo wa kuchambua kauli wanazozitoa hali ambayo inawapasa wawe makini.

Wakati tukisisitiza wananchi kuzingatia amani katika kipindi hichi tete, tayari watu watatu wakaazi wa Kangagani kisiwani Pemba hivi karibuni wameripotiwa kujeruhiwa ikisemekana kushambuliwa kwa mapanga.

Mengi yamesemwa na yanaendelea kusemwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na kushambuliwa kwa watu hao, hata hivyo kwa upande wetu kilichotokea Kangagani hatukinasibishi na hayo yaliyosemwa.

Kwenye mitandao hiyo wapo wanaolinasibisha suala hilo na itikadi za siasa na wapo wengine wanalinasibisha tukio hilo na imani za dini, hasa kwa kile kinachosemekana kuwa wameshambuliwa wakiwa ndani ya msikiti.

Kama tulivyosema kwa upande wetu suala hili hatulinasibishi na masuala ya dini wala siasa, kwa sababu kwenye dini ya kiislamu ambayo inawafusi wengi hapa Zanzibar, inakaza kabisa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia.

Aidha hata kwenye siasa za mfumo wa vyama vingi ambayo tumeianzisha kwa sheria za nchi yetu, hakuna kifungu chochote kinachoruhusu mtu kutoka chama kimoja kumshambulia wa chama chengine.

Kwa hiyo, tukio lililofanyika Kangagani halina shaka kuwa ni uhalifu, hivyo aliyefanya au kikundi kilichoratibu kutekelezwa kwa shambulizi hilo kinapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Ni vyema jeshi la polisi ambalo linajukumu la kulinda raia na mali zao, likahakikisha linachunguza vizuri tukio hilo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria waliohusika, ni kwa kufanya hivyo Jamhuri itakuwa imewapa haki walioshambuliwa.

Wakati huu tukielekea kwenye uchaguzi mkuu tusingependa matukio kama haya ya kihalifu yanajitokeza kwa sababu wale wanaoyahusisha na siasa wanaweza kupata nguvu za hoja zao.

Pia hatuamini waislamu wenye kuabudia Mungu mmoja, Mtume wao mmoja, kitabu chao kimoja wanaweza kuvukwa na imani kiasi cha kuwashambulia waumini wengine wasio na hatia.

Tunadhani huu ni wakati wa wanasiasa kupunguza jazba na kuwaeleza wafuasi wao kwamba wazanzibari wanataka amani na kiukweli wasingependa kujitokeze viashiria ambavyo vinaweza kuchochea na kuvuruga utulivu na kutuletea mifarakano.

Ukweli ni kwamba kama wananchi wakitakiwa wachague baina ya uchaguzi na amani, wengi wao watachagua amani kwa sababu ndiyo inayowahakikishia utulivu katika maisha yao na kufanya shughuli zao bila ya hofu.

Zanzibar ya uchaguzi wa amani inawezekana, Zanzibar bila ya uhalifu inawezekana.