NA HUSNA SHEHA
OFISI ya dawati na jinsia ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, inatoa mafunzo ili kuweza kusaidia jamii kudhibiti janga la udhalilishaji katika jamii.
Mkuu wa dawati hilo, Fatma Juma Mohammed akizungumza na Zanzibar leo, alisema kila mwaka wanapokea wanafunzi 30 kutoka katika vyuo tofauti kwa kuwapatia mafunzo hayo kikiwemo cha Mwalimu Nyerere ili kuweza kujua elimu ya kuvipinga vitendo hivyo.
Alisema dawati ni chombo kilichoanzishwa kwa lengo la kusimamia na kushuhulikia kesi za wanawake na watoto na serikali ilianzisha kutokana kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji katika nchi ya Tanzania.
Hata hivyo alibainisha kuwa udhalilishaji ni kitendo anafanyiwa mtu awe kwa ridhaa au bila ya ridhaa yake na kupelekea madhara ya kimwili, kiakili, kihisia na kisaikolojia.
Mkuu huyo alisema mafunzo hayo kwa mwaka huu yameanza Septemba 15 , mbali ya wanafunzi hao kutoka vyuoni pia wanapokea wanafunzi kutoka taasisi za serikali wa halmashauri ya Wilaya kutoka kitengo cha mtambuka wanaohusiana na udhalilishaji.
Aidha alisema kuna wanafunzi saba ambao waliotoka katika taasisi hiyo ambao wamemaliza mafunzo hayo Septemba 24.