NA HAFSA GOLO

WAKATI Kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu zikiendelea, wanafunzi wametakiwa kuzingatia masomo yao badala ya kujiingiza katika masuala ya siasa.

Mkurugenzi wa idara ya elimu sekondari katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Asya Iddi Issa, alisema hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Mazizini.

Asya Iddi Issa,

Alisema wanafunzi kujiingiza kwenye siasa kunaweza kuwatoa nje ya masomo jambo linaloweza kusababisha kupata matokeo mabaya katika mitihani yao ya taifa.

Aliwataka wanafunzi hasa wa kidatu cha nne kuzidiasha bidii ya masomokwa kuwa muda uliobakia ni mfupikabla ya kufanyika kwa mitihani ya taifa.

 “Wanafunzi nawaomba wabaki katika nafasi zao za masomo huku wakiongeza juhudi na sio kufuata shangwe za kisiasa watambue elimu ndio msingi wa maendeleo na kutimiza ndoto zao,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema uzoefu unaonesha kwamba wanafunzi kipindi kama hiki wanafunzi wengi hushiriki katika kampeni na wengine huthubutu hata kuvaa kinyume na mila na desturi za Mzanzinbari.

Hivyo aliwashauri wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao katika kipindi hichi ili kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa kuondokana na ukiukwaji wa maadili hasa ikizingatiwa wao ni wanafunzi.

Aidha aliwasihi walimu kuacha kuhubiri siasa wanapokuwa kazini badala yake wajikite katika usomeshaji ili kuleta ufaulu wa kiwango kinachoridhisha katika masomo yao wanayofundisha.

Aliwahimiza watumishi hao kuhakikisha wanazingatia sheria ya utumishi wa umma sambamba na kuwa makini katika suala zima la uwajibikaji wa majukumu yao.