NA ASYA HASSAN
MWENYEKITI wa mtandao wa jinsia Zanzibar, Asha Aboud Mzee, amesema ipo haja kwa Zanzibar kuanzisha chuo cha siasa ambacho kitaweza kuwajenga wanawake kujiamini na kuwa na uthubutu wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Alisema uwepo wa chuo hicho kitasaidia kuwapika wanawake hao na kuweza kujiamini katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pale unapofika uchaguzi mkuu.
Mwenyekiti huyo alisema hayo huko Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, alipokuwa katika mkutano wa kuangalia changamoto zilizojitokeza kipindi cha kushajihisha jamii kugombea nasfasi hizo.
Alisema wapo wanawake wanauwezo lakini wanashindwa kugombea kutokana na hawana elimu na hawajiamini, hivyo kuwepo kwa chuo hicho itakuwa chachu ya kuwawezesha kugombea nafasi hizo.
Mwenyekiti huyo, alisema licha ya taasisi mbalimbali, ikiwemo Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzani, Zanzibar (TAMWA), kuhamasisha wanawake hao kujitokeza lakini msukumo unahitajika zaidi ili kuweza kufikiwa kwa lengo la 50 kwa 50.
Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuvitaka vyama vya siasa kuangalia mfumo wa vyama vyao kwa kutoa nafasi kubwa wanawake kuchukua nafasi ya uongozi.
Kwa upande Afisa miradi kutoka TAMWA, Sabrina Yussuf Mwintanga, alisema wameweza kuwafikia asilimia kubwa ya wanawake kuwapa elimu juu ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Alisema hali hiyo imeweza kuwafanya wanawake wengi kujitokeza katika kuchukua fomu hizo, lakini changamoto kubwa bado ipo kwa baadhi ya vyama vya siasa hawakuyarudisha majina hayo.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo walisema elimu zaidi inahitajika kwa vyama vya siasa, kwani baadhi yao bado vinamfumo dume.
Mbali na hayo walisema pia asilimia kubwa ya wanawake wanahitaji kuchukuwa fomu kwa ajili ya kugombea lakini wanashindwa kutokana na kipato kidogo.