BAMAKO,MALI

KIONGOZI wa wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Mali, Kanali Assimi Goita ametangaza kuunga mkono mpango wa kuundwa Serikali ya mpito ya miezi 18 na kuahidi kurejesha utawala wa kiraia baada ya kipindi hicho.

Kundi la wataalamu lililoteuliwa na wanajeshi hao waliofanya mapinduzi limepanga kuongoza nchi ya Mali kwa muda wa miezi 18 ambapo mkuu wa Serikali hiyo atakuwa mwanajeshi au raia.

Kanali Assimi Goita alisema,walitoa ahadi madhubuti kwamba hawatobakisha juhudi yoyote ya kuhakikisha mambo hayo yanatekelezwa kwa manufaa ya watu wa Mali.

Rais wa mpito atachaguliwa na wapiga kura watakaoteuliwa na wanajeshi.

Hayo yalisemwa na Moussa Camara,msemaji wa wanajeshi waliofanya mapinduzi.Matamshi hayo aliyatoa mwishoni mwa siku tatu za mazungumzo.

Muungano wa M5-RFP ulioongoza maandamano dhidi ya Rais Ibrahim Boubacar Keita kabla ya mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 18, 2020, ulipinga vikali jambo hilo hasa suala la mwanajeshi kuongoza Serikali ya mpito.

Hata majirani wa Mali nao walipinga suala hilo wakisisitiza kuwa Serikali ya mpito haipaswi kuwa zaidi ya mwaka mmoja.

Hivi karibuni pia, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) iliwataka wanajeshi wafanya mapinduzi huko Mali kumtangaza rais mpya wa mpito wa nchi hiyo kufikia Septemba 15.

Taarifa iliyotolewa na Ecowas ilisisitiza kuwa, Rais na Waziri Mkuu wa mpito wa Mali watakaotangazwa katika kipindi cha wiki moja ijayo sharti wawe raia.

Kadhalika jumuiya hiyo ya kikanda yenye nchi wanachama 15 ilibainisha kuwa, vikwazo ilivyotangaza dhidi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi vitaendelea kuwepo hadi pale viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali watakapokabidhi madaraka kwa Serikali ya mpito ya kiraia.