NA LAILA KEIS

WANANCHI wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ wametakiwa kujitokeza kupima Malaria, ikiwa ni moja kati ya mpango wa serikali katika kutokomeza maradhi nchini.

Mkurugenzi Msaidizi Manispaa ya Wilaya ya Magharibi ‘B’, Leyla Salum Ali, aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili Ofisini kwake Kwamchina Mjini Unguja.

Alisema zoezi la upimaji ni moja ya ajenda ya serikali katika kutokomeza maradhi hayo nchini, ambapo zoezi hilo limeanza katika shehia ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, wameamua kuwapima wananchi wa maeneo hayo kutokana na uchunguzi walioufanya kupitia vituo vya Afya, na kugundua kuwa shehia hiyo ina wagonjwa wengi wa malaria.

Aidha alisema, katika zoezi la upimaji wa awamu ya kwanza jumla ya wagonjwa 33 kati ya watu 3,017 waliopimwa waligundulika kuwa na malaria na awamu ya tatu waliopimwa walikua ni 4,517, ambapo 18 waligundulika kupata malaria.

“Kila awamu tunapata wagonjwa wengine tofauti, hii inaonesha kuwa Malaria bado ipo na wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari ya hali ya juu ikiwemo kusafisha mazingira yanayowazunguka ili kuondoa mazalia ya mbu,” alisema.

Sambamba na hayo alisema zoezi hilo litakuwa endelevu kwa shehia ambazo zitaonesha kutoa wagonjwa wengi wa malaria kwa kuzipa kipaumbele.

Hata hivyo, alisema baadhi ya wananchi bado ni wazito kujitokeza kupima, hivyo aliwataka wananchi kutoa ushirikiano wao, ili kuisaidia serikali kutokomeza Malaria nchini na kutumia vyandarua vinavyotolewa na serikali katika kutokomeza ugonjwa huo.

Mmoja ya wananchi wa shehia hiyo waliojitokeza kupima afya zao Fatma Mahmoud, aliishukuru serikali kwa kufanya zoezi hilo, kwani wananchi wengi hawana utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.

“Watu tunasubiri mpaka ugonjwa utuangushe ndio tukimbilie hospitali, hatuna utaratibu wakuchunguza afya zetu, hii ni fursa nzuri kwetu kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zetu mara kwa mara, ili pale tunapogundulika tuweze kupatiwa matibabu mapema,” alisema.

Sambamba na hayo aliwataka wananchi kutodharau maagizo ya serikali na badala yake wajitokeze kupima, ili kutokomeza janga hilo.