ARAFA  MOHAMED

WANANCHI wa Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’Mkoa wa Kaskazini Unguja,wameishukuru Serikali pamoja na mfuko wa maendeleo TASAF katika Mkoa huo ,kwa kuwajengea jengo la Skuli kwa lengo la kupunguza tatizo la wanafunzi wengi kusoma katika darasa moja.

Hayo yalielezwa na wakaazi  wa eneo hilo walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari huko kijijini kwao Mahonda Kaskazini Unguja.

Walisema,wanafunzi wa skuli ya Mahonda wamekuwa wanapata tabu sana kutokana na uhaba wa madarasa, lakini kwa sasa wanashukuru kuona jengo linajengwa wanatarajia tatizo la Wanafunzi wengi kusoma katika darasa moja na wengine kusoma nje litapunguwa.

Shulu Khamis Kombo, mmoja wa wakaazi katika kijiji hicho alisema, kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiomba kuongezewa jengo la skuli ili watoto wao waingie skuli hapo kwa wakati mmoja,nasio kuingia kwa zamu kutokana na kuhofia kutokea vitendo vya udhalilishaji.

“Tumefurahi sana kujengwa kwa jengo hili kutokana na hivi sasa wanafunzi wanaingia kwa awamu mbili asubuhi na jioni, kwasababu kuna uhaba wa madarasa kuwa kidogo kwa hivyo  tunataka waingie wote wakati mmoja lengo letu linaweza kutimia, biashara asubuhi jioni kuhesabu mapato”alisema.