TUNAAMINI kuwa elimu ni hazina na aliyesoma si sawa na asiyesoma. Maneno haya tunataka kuyanasibisha na matatizo mengi yanayotokea hasa katika upotevu wa rasilimali asili muhimu kabisa duniani.
Upotevu wa vyanzo vya maji, hili ni tatizo linaloikabili dunia kwa sasa ambalo linatokana na sababu kadhaa zikiwemo zinazoababishwa na nguvu na maarifa ya kibinadamu sambamba na majanga ya kimaumbele.
Wanaadamu wamekuwa wabunifu maradufu katika dunia ya teknolojia.
Wanaweza kubuni zana za kimaendeleo lakini zinazoleta athari kwa watu na mazingira. Wakati mwengine uvumbuzi huo hauzingatii athari hizo ila hufanywa kwa kukidhi matwaka ya teknolojia ambayo hubadilika kila baada ya miezi 18.
Kwa upande wa teknolojia, zipo kwa mfano zana nyepesi tu ambazo hutumia kuharibu mazingira kama vile misumeno ya moto kwa ajili ya kukatia miti bila mpango maalum. Miti hiyo hutumiwa kwa ajili ya kutengeneza makaa, nguzo za umeme, kujengea, na matumizi mengine ya kibinadamu.
Katika kutimiza mahitaji ya watu yanayokua kwa kasi. Ukataji wa miti kwa mfano, hupunguza kiwango cha hewa safi, miti inanyonya hewa chafu na kutoa hewa safi ambayo tunaihitaji kwa matumizi wetu.
Matokeo yake kiwango cha joto hongezeka na kuharibu mifumo mingine ya hewa. Hali hii huchangia kutokea majanga ya kiasili kama vile mvua kubwa na mafuriko, maporomoko ya udongo au matope, ukame unaosababisha njaa na majanga mengine.
Wakati dunia ilipokuwa mstari wa mbele kuhifadhi mazingira jamii ilishajiika na kampeni ya ‘kata mti panda miti’ wala hakukuwa na malalamiko ya upotevu wa vyanzo maji tunayoyashuhudia sasa.
Wimbo huu ulitekelezwa kwa vitendo na kila mmoja alijua umuhimu wa kuotesha miti. Lakini binadamu tunahitaji kukumbushwa juu ya mambo ambayo ni faida ili kuepusha athari zinaoweza kuwakumba wengine hata wasiohusika.
Haya yanaweza kuleta matokeo ya mabadiliko ya mambo mengi sana ambayo miongoni mwao tukashindwa kuyatekeleza ingawake mawazo yake yalikuwepo tokea zamani. Ili kupunguza ongezeko la watu duniani watu washajiishwe kufuata kanuni za uzazi salama kurahisisha huduma zao kwa mujibu wa mahitaji yao.