NA KHAMISUU ABDALLAH
WANANCHI wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wamemuomba mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kulifanyia kazi suala la vitendo vya udhalilishaji pindi atakapochaguliwa ili kulinda nguvu kazi ya taifa.
Ombi hilo walilitoa mara baada ya mgombea huyo kufika katika mkoa huo ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya kukutana na makundi mbalimbali kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi.
Walisema, pamoja na serikali ya awamu ya saba kutunga sheria, bado wapo baadhi ya watu wanaowadhalilisha wanawake na watoto.
Walisema pamoja na kesi hizo kufikishwa mahakamani bado hukumu inayotolewa kwa wahalifu haikidhi haja kutokqna na madhara wanayoyapata waathiriwa wa vitendo hivyo.
Mmoja ya wananchi hao Mekrida Masato Lutema mkaazi wa Kinyasini, alisema mkoa huo unaongoza kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa watoto hali ambayo inaondosha matumaini ya watoto katika kupata elimu na kuathirika kisaikologia.
NaYe Mtumwa Mkwaju Mnubi alisema pamoja na serikali kutaka kesi hizo kufikishwa katika vyombo vya sheria lakini wapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakizimaliza kesi hizo kifamilia kwa kutaka kupewa pesa hivyo ni lazima changamoto hizo zirekebishwe ili kukomesha matukio hayo.
“Tukumbuke kuwa pesa haitaondosha maumivu ya mtoto, hivyo tunaomba ukiingia ikulu utuangalie kwa jicho la huruma hasa suala hili ambalo limekuwa likituathiri sana na watoto wetu,” alisema.