NA BAHATI HABIBU

WANANCHI wa Jimbo la Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, wameipongeza serikali kwa kuwapatia miradi mbali mbali ya maendeleo katika Wilaya ya Kati na  wamemuomba mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa Chama cha Mapinduzi kuwatembelea ili kufahamu changamoto zao.

Wamesema kuwa katika jimbo la Tunguu  wamehabatika kuwa na majengo mengi ya Serikali ikiwemo jengo la Mahakama Kuu , Vyuo Vikuu    Ofisi za Uhamiaji ,  Bunge na Hospitali inayojengwa katika kijiji cha Binguni.

Hayo wameyasema kwenye mkutano wa hadhara ya kuwatambulisha wagombea wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Chama Cha Mapinduzi uliofanyika katika viwanja vya halmashauri vilivyopo Tunguu.

‘’ Tumefurahishwa na maendeleo aliyoyaleta Dk. Shein ya kutujengea jengo la Mahakama Kuu na Hospitali ya aina yake iliopo Binguni vitu ambavyo vitazidi kulifanya Jimbo hilo kutambulika kimataifa ’’ walisema wananchi hao.

Aidha wamedai katika eneo linalojengwa Mahakama Kuu baada ya kubomolewa nyumba kuna visima na mashimo ya makaro ambayo yapo wazi hivyo wameiomba Serikali kuyafukia kwani yanahatarisha usalama wa watoto wao na mifugo yao.

Nae mgombea Ubunge Khalifa Salum Suleiman wa jimbo hilo ameahidi kuwa atashirikiana na Serikali ya chama Cha Mapinduzi, ili tatizo la Maji, Umeme  na Miundombinu ya Barabara za ndani kwa kuziwekea fusi na kuwa hayo yatabaki kuwa ya historia katika jimbo hilo.

Kwa upande wa mgombea Uwakilishi amewataka wanachama wa C.C.M na Wananchi kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi kuanzia  ngazi ya Wadi, Jimbo, Uraisi wa Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huo ni muendelezo wa kutekeleza  mpango mkakati wa chama hicho wa kupiga kampeni nyumba kwa nyumba, ili kuhakisha chama cha Mapinduzi kinapata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka huu.