MINSK,BELARUS

TAKRIBAN wanawake elfu kumi wamefanya maandamano katika mji wa Minsk wakitaka kujiuzulu kwa rais wa nchi hiyo Alexander Lukashenko katika siku ya 35 mfululizo wa maandamano makubwa dhidi ya serikali.

Waandamanaji hao walibeba picha za Maria Kolesnikova,kiongozi wa baraza la uratibu la upinzani linalotaka kuandaliwa kwa uchaguzi mpya wa urais katika taifa hilo lililokuwa la muungano wa kisovieti, aliyefungwa gerezani baada ya polisi kujaribu kumfurusha kwa lazima kutoka nchini humo.

Waandamanaji wengine walibeba mabango yaliokuwa yameandikwa ”ulipaka moyo wangu na machungu ya samawati” wakimaanisha madai ya Lukashenko kwamba awali baadhi ya wanawake walijipaka rangi kuonyesha kuwa walipata majeraha baada ya kupigwa na polisi.

Kundi la kutetea haki za binadamu la Viasna, limesema kuwa zaidi ya watu 70 walikamatwa wakati wa maandamano hayo.

Lukashenko alikataa kukutana na baraza hilo na viongozi wengi walizuiliwa ama kuondoka nchini humo.