NAIROBI, Kenya
BAADA ya kuiongoza Kenya kushiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri kwa mara ya kwanza tangu 2004, nahodha Victor Wanyama, sasa ana malengo mapya Harambee Stars.

Nyota huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs amesema hana nia ya kutundika daluga katika soka ya kimataifa hivi karibuni, na kubwa zaidi katika malengo yake ni kuongoza Kenya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Lakini haitakuwa kazi rahisi kufanya hivyo kwani Harambee Stars italazimika kuzifunga Mali, Uganda na Rwanda na kuibuka kileleni mwa kundi ‘E’ katika safari ya kujikatia tiketi ya kutua Qatar.
Wanyama amesema wapo kwenye kundi gumu na wanaheshimu kila kikosi, lakini, badala ya kuongopa timu nyingine wanatakiwa kujifua vilivyo na kuwabwaga kwa sababu hakuna lisilowezekana katika soka.(Goal).