LONDON,UINGEREZA

WAPATANISHI wa Umoja wa Ulaya wamesema kwamba wako tayari kuandaa makubaliano ya kisheria juu ya biashara baina ya Umoja huo na Uingereza, muda mchache kabla ya mazungumzo baina ya pande hizo mbili kurejea kwenye majadiliano.

Gazeti la The Times limeandika kwamba mkuu wa timu ya upatanishi ya Umoja wa Ulaya, Michel Barnier, yuko tayari kuifanyia kazi rasimu ya pamoja kuhusu makubaliano ya biashara huria wiki hii.

Mpatanishi huyo mkuu wa Umoja wa Ulaya alisema anatarajia mwenzake wa Uingereza, David Frost, atatowa taarifa za kina juu ya kiwango cha uvuvi kwa kila upande na sera ya baadaye ya ruzuku.

Gazeti hilo limeripoti kwamba kwa sasa Umoja wa Ulaya umeachana na kitisho cha kusitisha mazungumzo ya kibiashara na kiusalama na Uingereza.