NA RAYA HAMAD, WKS

MKURUGENZI Idara ya Msaada wa Kisheria Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said, amesema Wasaidizi wa Sheria wana umuhimu mkubwa katika jamii kutokana na kazi zao.

Aliyasema hayo katika mkutano wa pili wa robo mwaka wa kuratibu masuala ya msaada wa kisheria uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni.

Alisema jitihada wanazozifanya wasaidizi wa sheria zinahitaji kutambuliwa na kuthaminiwa ili kuwapa hamasa ya kuendelea kufanya vizuri.

Alieleza kuwa sheria ya msaada wa sheria imewatambua wasaidizi wa sheria kama ni watoa msaada wa kisheria hivyo wanahitajika kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Akisoma ripoti ya mwaka ya utekelezaji wa shughuli za idara, alisema imewafikia wananchi 338 wa shehia nne za Unguja kwa kuwapa elimu ya kanuni na sheria za msaada wa kisheria na kwa Pemba wamewafikia wananchi 150 katika wilaya ya Micheweni.

Alisema idara pia imekamilisha mfumo wa usajili kwa njia ya kielektroniki kwa watoaji wa huduma wa kisheria.

Alisema mfumo huo unawatambua watoaji msaada wa kisheria na kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi za watoa huduma.