NA MARYAM HASSAN

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi amewataka wasomi kutoa mapendekezo yao ya sera zenye kutekelezeka kwa serikali ijayo ili kuendeleza uchumi wa Zanzibar.

DK. Mwinyi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wasomi wa vyuo vikuu katika kongamano la wiki ya Elimu Zanzibar lililotayarishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali lililofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Tunguu wilaya ya Kati Unguja.

Alisema duniani kote wasomi ni tegemeo katika kutoa mapendekezo yanayofaa ya maendeleo ya nchi  na kwenye kukabiliana na changamoto zinazojitokeza hasa katika ajira.

Alisema matumaini yake kuwa wasomi wataendeleza sera zinazofaa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya serikali ijayo kuinua uchumi wa Zanzibar siku hadi siku.

“Zanzibar kuna vyanzo mbalimbali vya kuimarisha uchumi vikiwemo vya uvuvi, bandari, viwanda ambavyo vikitumiwa vizuri vitahakikisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi zaidi,” alieleza Dk. Mwinyi ambae pia ni mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi.

Alisema ni jukumu la wasomi kutoa mapendekezo kwa serikali jinsi gani ya kuweka sera na sheria zitakazochochea na kukuza uchumi wa nchi kupitia dhana ya uchumi wa buluu ili kutatua tatizo la ajira linaloikabili jamii.

Alieleza kuwa endapo wananchi wa Zanzibar watamchagua kuwa Rais wa Zanzibar, ataunda serikali sikivu itakayoendeshwa kwa kufuata maelekezo na ushauri wa wataalamu.

Aidha aliahidi kutekeleza kwa vitendo ahadi anazozitoa na kubadilisha tabia za watu kufanya kazi kwa mazowea badala yake atahakikisha wanawajibika kutokana na nafasi zao kuanzia ngazi za juu hadi za chini katika serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya serikali.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa elimu na ndio maana wana kila sababu ya kusherehekea kupitia makongamano mbalimbali yanayofanyika nchini.

Mbali na hayo, alimpongeza mgombea huyo, kwa kuonesha moyo wa kuthamini jitihada za elimu nchini.