ROMA,ITALIA

MATOKEO ya kura ya maoni iliyopigwa Italia yanaonyesha kuwa raia wengi wa nchi hiyo wanataka kupunguzwa kwa idadi ya wajumbe katika mabaraza mawili ya bunge nchini humo.

Takwimu za awali za matokeo hayo zilionyesha kuwa asilimia 70 ya wapiga kura waliridhia kupunguzwa kwa theluthi moja ya wabunge.

Mpango uliopo ni kupunguza idadi ya wabunge katika baraza la wawakilishi kutoka 630 hadi 400, na kutoka 315 hadi 200 katika baraza la seneti.

Vuguvugu la Nyota tano linaloongozwa na Waziri wa mambo ya nje Luigi Di Maio ndilo linaloongoza miito ya mageuzi hayo.

Na katika uchaguzi wa jimbo la Tuscany uliofanyika sambamba na kura hiyo ya maoni, chama cha mrengo wa kushoto kimeweza kudumisha wingi wake dhidi ya chama cha mrengo mkali wa kulia kinachoongozwa na naibu waziri mkuu wa zamani, Matteo Salvini.