KINSHASA,CONGO

WATU wasiopungua 58 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio ya wanamgambo wa ADF wa Uganda katika mkoa wa Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hayo yalielezwa na Adjio Gidi,Waziri wa Mambo ya ndani wa DRC na kuongeza kuwa, idadi kubwa ya watu katika maeneo yaliyoshambuliwa walikimbia makaazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.

Alisema ADF iliua watu 23 katika eneo la Irumu kusini mwa mkoa wa Ituri  na kisha ikaua watu wengine 35 katika eneo hilo siku iliyofuatia.

Mmoja wa wakaazi wa kijiji chenye misitu mikubwa cha Tshabi mkoani hapo amenukuliwa na duru za habari akisema kuwa,wanamgambo hao walitumia bunduki,visu,mapanga na silaha nyengine katika mashambulio hayo.

Mapema mwezi Juni mwaka huu, watu 16 waliuawa na ADF mkoani Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo wakiwemo watoto watano wa kike, wiki chache baada ya genge hilo kuua watu wengine 17 katika hujuma tofauti mkoani hapo.

Maelfu ya Wacongo waliuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa ADF ambao asili yao ni Uganda hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi,tokea mwaka 2014.

Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maofisa usalama kwa upande mwengine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.