MOGADISHU,SOMALIA

MSEMAJI wa Serikali ya Somalia amesema kuwa watu, watatu akiwemo mtoto moja, wameuawa na wengine saba kujeruhiwa katika shambulio la bomu la kujiripua lililotekelezwa ndani ya mgahawa huko Mogadishu.

Msemaji wa Wizara ya Habari ya Somalia, Ismail Mukhtar alisema kuwa, mtu aliyefanya shambulizi hilo aliingia ndani ya mgahawa wa Blue Sky karibu na Makumbusho ya Taifa kabla ya kujiripua mwenyewe.

Alisema kuwa,gaidi huyo aliyekuwa na nia ya kuwauwa raia,alijiripua ndani ya mgahawa huo na kusababisha vifo vya raia watatu na kujeruhi wengine saba.

Mtu mmoja aliyeshuhudia shambulio hilo aliyejulikana kwa jina la Kasim Ali alisema kuwa,mripuko huo ulikuwa mkubwa na kwamba aliwaona watu wakikimbizwa Hospitali baada ya kujeruhiwa huku baadhi yao wakiwa mahututi.

Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la kujiripua kwa bomu.

Kundi la al Shabab lenye makao yake nchini Somalia ambalo lina muungano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida, mara kwa mara limekuwa likihusika na mashambulizi dhidi ya raia na maeneo ya Serikali mjini Mogadishu.