NA ASIA MWALIM

IDARA ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar, imesema itashirikiana na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) na Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki ya kupiga kura kwa usalama kama ilivyo kwa watu wasio na ulemavu.

Mkurugenzi wa idara hiyo, Abeda Rashid Abdalla aliyasema hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Migombani, Zanzibar.

Mkurugenzi huyo alisema watu wenye ulemavu mara nyingi huacha kujitokeza kwenye vituo vya kupigia kura wakati kupiga kura ni haki yao ya msingi.

Alisema idara hiyo imekua ikishiriki mikutano mbalimbali ya tume za uchaguzi na kutoa maoni yao kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki ya kuchagua na kupewa kipaumbele kwenye suala hilo.

Alifahamisha kuwa serekali inatambua umuhimu na kuwaamini watu wenye ulemavu ni sehemu katika jamii hivyo imetoa muongozo kila taasisi kuandaa miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi Abeda alieeza kuwa katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, idara itahakikisha kutakuwa na muongozo madhubuti wa maeneo yatakayotumika kipindi cha uchaguzi ili kuhakikisha mazingira ya kupiga kura yanakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu.

“Katika kuhakikisha usalama wa watu wenye ulemavu, tunahitaji kupewa vitambulisho maalum vitakavyotumika kama utambulisho wetu ili kupata huduma kwa haraka tunapofika vituoni,” alisema.