KINSHASA, DRC

MAMLAKA ya jimbo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema takribani watu 50 wanahofiwa kupoteza maisha baada ya kuporomoka kwa mgodi wa madini ya dhahabu, mashariki mwa taifa hilo.

Mkasa huo ulitokea jana katika eneo la machimbo holela ya watu, huko mjini Kamituga katika jimbo la Kivu ya Kusini, ikielezwa kusababishwa na mvua kubwa katika eneo hilo.

Wakati Gavana wa Jimbo Theo Ngwabidje alisema idadi ya waliokufa ikifikia 50, na wengi wao wakiwa ni vijana, Meya wa mji wa Kamituga Alexandre Bundya anasema bado hawajawa na uhakika wa idadi kamili ya watu walioathirika katika ajali hiyo ya kuporomoka kwa mgodi.