NA KHAMISUU ABDALLAH

WATU wawili wamefikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe wakikabiliwa na shitaka la wizi wa vespa.

Washitakiwa hao ni Issa Suraka Amour (25) mkaazi wa Darajabovu na Ali Abdalla Ali (30) mkaazi wa Kwamtipura wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambao wote kwa pamoja walifikishwa mbele ya Hakimu Suleiman Jecha Zidi.

Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai kwa kushirikiana na Koplo Salum Ali walidai kuwa washitakiwa hao walipatikana na kosa la wizi kinyume na kifungu cha 267 (1) na kifungu cha 274 (2)(c) vya sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Walidaiwa kuwa April 28 mwaka huu saa 1:00 usiku huko Bububu Mwanyanya kwa pamoja waliiba vespa aina ya DV yenye namba za usajili Z 794 JT rangi nyekundu na baadae waliibadilisha namba za usajili kuwa Z 628 JS.

Pia washitakiwa hao walidaiwa kuchukua pesa shilingi 1,500,000 zilizokuwemo kwenye vespa hiyo mali ya Said Sheha Khalfan kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mahakama ilikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.