NA LAILA KEIS

WATU wawili wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani zilizotokea katika maeneo tofauti ya mkoa wa Mjini Magharibi.

Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi Awadhi Juma Haji, alieleza hayo kwa waandishi wa habari alipokua akitoa taarifa kwa matukio ya wiki ofisini kwakwe Mwembemadema, Unguja.

Kamanda Awadhi alimtaja mmoja ya marehemu hao kuwa ni Ismail Shaban Hanya (28) mkaazi wa Fuoni, wilaya Magharibi ‘B’, aliekuwa akiendesha pikipiki yenye namba za usajili MC 474 XR akitokea Buyu kuelekea Mbweni alishindwa kuiongoza vyema pikipiki na kupelekea kugonga ukuta wa nyumba alipofika maeneo ya skuli ya Laurent.

Aidha alitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva kwa kwenda mwendo kasi na kutokuwa makini wakati wa kuendesha chombo cha moto barabarani hali iliyosababisha kupelekea kifo chake.

Awadh alisema mwendesha pikipiki huyo, alipata majeraha sehemu ya kichwa na kupoteza damu nyingi, hali iliyopelekea kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu huko hospitali ya Mnazimmoja.

Aidha Kamanda alieleza ajali nyengine ya gari aina Sino iliyosababisha kifo cha Masoud Choum Juma (60), mkaazi wa Donge, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Septemba 17, mwaka huu majira ya saa 3:30 asubuhi, maeneo ya Chuini katika barabara ya Mfenesini kuelekea Bububu na kumgonga dereva wa pikipiki yenye nambari za usajili Z 953 AL aina ya Yamaha.

Alieleza kuwa, gari iliyosabisha ajali hiyo ni aina ya Sinoo yenye nambari za usajili T 788 DGT, iliyokuwa ikiendeshwa na Tresifori Bahati Jumwensi (41) mkaazi wa Kiwengwa, wilaya ya Kaskasini ‘B’ mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari ambae alirudi nyuma bila ya tahadhari na kumgonga mpanda pikipiki ambae alianguka chini na kumkanyaga kichwani kwa gari hiyo.

Aidha alisema jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa Tresifori, hivyo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo.