NA KHAMISUU ABDALLAH

MWENDESHA Mashitaka Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Said Ali ameiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi inayowakabili washitakiwa wanne wakiwemo wawili ndugu wa familia moja tayari umeshakamilika.

Hatua hiyo imekuja baada ya washitakiwa hao kukataa makosa yao ikiwemo la kuiba gari aina ya DYNA mali ya Ibrahim Abdalla Yussuf.

Washitakiwa hao ni Ibrahim Mgeni Zisi (28),Khamis Mgeni Zisi (37) wote wakaazi wa Magombeni, Mzee Ali Mzee (50) mkaazi wa Jumbi na Khamis Shafi Khamis (50) mkaazi wa Fuoni Kibondeni.

Washitakiwa hao walifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu mdhamini wa mahakama hiyo Mohammed Subeit ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walipatikana na makosa ya wizi.

Ilidaiwa kuwa kosa la kwanza walilopatikana nalo washitakiwa hao ni wizi kinyume na kifungu cha 251 (1) (2) (a) na kifungu cha 251 (a) (2) (a) na 258 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Walidaiwa kuwa Machi 19 mwaka 2019 saa 10:00 jioni huko Tomondo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, wote kwa pamoja waliiba gari aina ya DYNA yenye namba za usajili Z 812 BY yenye thamani ya shilingi 7,000,000 mali ya mlalamikaji Ibrahim Abdalla Yussuf kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Kosa la pili walilopatikana nalo washitakiwa hao ni kuharibu mali kwa makusudi kinyume na kifungu cha 326 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.