KWA kawaida mchakato wa uchaguzi huambatana na shughuli mbalimbali, nyengine hutekelezwa kwa mujibu wa sheria na nyengine kwa mujibu kanuni, ambazo zote hizo lengo lake ni kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.

Moja ya mchakato muhimu kwenye uchaguzi mkuu ni kampeni, ambapo katika hatua hii vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea huruhusiwa kuwatambulisha wagombea waliowasimamisha sambamba na kunadi sera na ilani zao.

Katika hatua hii hutegemea chama kilivyojipanga lakini Tume za uchaguzi huviruhusu vyama vipige kampeni kadiri vinavyoweza kwa kupita katika kwenye vitongoji, vijiji, shehia, majimbo, wilaya, mikoa na kukusanya watu wa nzima kama wanaweza.

Hatua ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu ni muhimu sana kwani hutoa fursa wananchi kusikiliza, kufahamu na kuchambua sera, ilani na ahadi zinazotolewa nwa wagombea na vyama vyao.

Bila shaka mwananchi kama mpiga kura baada ya kufahamu, kuelewa, kuvutika, kushawishika na sera, ilani na ahadi za wagombea na vyama vyao, ndipo inapochukua hatua za kufanya maamuzi siku ikifika akatumbukize kura yake katika chama kipi.

Hata hivyo, mchakato huu muhimu wakati mwengine hutawaliwa na mizengwe na hila nyingi na kwamba vyama na wagombea wasipochukua tahadhari nchi inaweza kuelekea kwenye machafuko.

Kampeni zisipofanywa kistaarabu ambapo kila mgombea anapopata fursa ya kupanda jukwaani badala ya kueleza sera yeye hutukana wagombea ama vyama vyengine kwa maneno makali, kushutumu, kupandikiza chuki na ubaguzi miongoni mwa wananchi, nchi yetu itaelekea kubaya na kukaribisha machafuko.

Tunavyoelewa maana ya kampeni za kisiasa ni kuwashawishi ama kuwabembeleza wapiga kura wakubaliane na sera ama ilani ya chama chako ili chama hicho ama mgombea wake wampigie kura.

Kampeni sio fursa kwa vyama na wagombea kushambulia wengine, kuwashutumu, kuwatukana, kuwagawa wananchi kwa misingi ya kiimani ama kuwafarakanisha.

Jukumu na wajibu wetu ni kutanabahisha, endapo tahadhari isipochukuliwa tukaruhusu kila mwenye lake binafsi dhidi ya mwengine aliseme kwenye kampeni, hatuombi lakini bila shaka tutaipeleka nchi tusikokutaka.

Tunaposema kwa msisitizo kuvitaka vyama na wagombea wafanye kampeni za kistaarabu maana yake yale watakayoyasema watakapisimama majukwani yalenge kuwaeleza wananchi vipi watawaletea maendeleo na vipi watazitua changamo zinazowakabi wananchi.

Tunaiomba sana serikali kwa kutumia vyombo vyake vya dola kamwe na kwa vyovyote isiwastahamilie wale wasio na dhamira ya kufanya kampeni za kistaarabu, kwa sababu wana dhamira ya kuharibu amani na utulivu uliopo.

Uchaguzi ni mchezo wa kisiasa na kila mchezo una sheria zake, hivyo kwenye kampeni tuhakikishe wagombea na vyama wasijaribu kuziamsha hisia za wengine, kampeni ziwe za kutibu majeraha, kampeni zizidishe mapenzi miongoni mwa wananchi.

Tukumbuke kuwa Zanzibar ni nchi ya wazanzibari wote, siku moja ya uchaguzi itapita, lakini maisha yatakuwepo baada ya siku hiyo na bila shaka baada ya uchaguzi tusalimiane tuwapongeze walioshinda na ni nafasi ya walioshindwa kujipanga.