NA KHAMISUU ABDALLAH

WIZARA ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto imewafungulia mashitaka wazazi wa watoto watatu waliopotea wiki moja iliyopita na kuhifadhiwa na serikali katika nyumba ya kulelea watoto Mazizini.

Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Shadya Mohammed Suleiman, alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kuwatembelea watoto hao huko Sebleni.

Alisema serikali haitawatoa watoto hao mpaka pale itakapowafikisha mahakamani na kuwachukulia hatua, ili iwe fundisho kwao na wazazi wengine.

Aidha alisema imeshazoeleka Zanzibar baadhi ya wazazi kuwatekeleza watoto na kuwatupa huku wakijua kwamba serikali itawachukua na baadae wanapewa wenyewe hivyo hivi sasa jambo hilo halitavumiliwa.

 “Hili suala la kuwatupa watoto limeshakuwa endelevu katika jamii sasa mara hii tunasema imeshatosha watoto hawa hatuwatoi mpaka tuone mahakama imechukua hatua dhidi ya kinamama wenye tabia hii ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema.

Hata hivyo, alifahamisha kuwa haingii akilini watoto watatu kupotea kwa wakati mmoja huku mzazi huna wasiwasi ukizingatia dunia imeharibika na vitendo vya udhalilishaji.

Naibu Shadya, aliwasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda watoto wao wakati wote na kuwakinga na matukio mbalimbali ikiwemo ya udhalilishaji wa kijinsia.

Sambamba na hayo, alisema imefika wakati kinamama kubadilika na badala yake kuweka mbele ulinzi wa watoto wakati wote kwani serikali inawahitaji katika ujenzi wa taifa la baadae.

“Wazazi wengi wameweka starehe mbele kweli tuna ukali wa maisha katika kutafuta riski lakini isiwe kisingizio cha kuwatekeleza watoto wetu haipendezi hawa ndio taifa la baadae ambalo litaongoza na kuleta maendeleo katika nchi yetu,” alisisitiza.        

Hivyo, aliwasisitiza ni wajibu wa kila mzazi kutenga muda mara kwa mara kuwatafuta watoto wao ili kujua kwamba wapo sehemu salama karibu na maeneo yao ili kuwakinga na vitendo viovu na majanga mengine.

Pili Sadallah Mussa ni mlezi wa nyumba ya kulelea watoto Mazizini alisikitishwa na jamii kutokuwa makini na malezi ya watoto wao ukizingatia dunia imeharibika na vitendo vya udhalilishaji.

Hivyo, alisema watoto hao wapo katika hali nzuri kiafya na kuisisitiza jamii kutowaachia watoto kuhangaika na kuwa karibu nao wakati wote.

Watoto hao walipokelewa katika nyumba ya kulelea watoto Mazizini Septemba 2, mwaka huu majira ya saa 11:30 za jioni ambao watoto wote hao wanatoka familia moja.