NA LAILA KEIS
JUMUIYA ya Wazee wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, imeeleza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anapaswa kushukuriwa kwa mengi mazuri aliyoifanyia jumuiya hiyo na wazee wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa muda, wa jumuiya hiyo iliyopo Makadara mjini Unguja, Ramadhan Suleiman Nzore alieleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili alipofika katika ofisi za sharika la magazeti ya Serikali Maisara.
Mwenyekiti huyo alisema wakati Dk. Shein akikaribia kukamilisha kipindi chake cha pili cha urais, atakumbukwa jinsi alivyohimiza umoja miongoni mwa wazanzibari, haki na usawa miongoni mwao.
Alisema katika kipindi cha miaka 10, kiongozi huyo mbali ya sharia na katiba ya nchi, aliitumia hekma na busara kujenga uchumi na ustawi wa jamii kiasi cha kukubali kuanzishwa kwa jumuiya zinazowaunganisha wanajamii.
Alisema jumuiya yao itaendelea kumshukuru Dr. Shein, kwa kuiwezesha kupata pembejeo za kilimo ambazo zimesaidia kutoa mazao bora katika bonde lao la cheju, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
“Tutaendelea kumkumbuka Rais wetu kipenzi kwa aliyotufanyia kwenye jumuiya yetu, yeye ni mzalendo na mwenye utu,” alisema.