MWASHUNGI TAHIR,   MAELEZO

WAZIRI wa Habari Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, ameitaka jamii kupatiwa elimu kwa lengo la kuwa na utaratibu wa kuweka  usafi katika mazingira wanayoishi.

Wito huo ameutoa huko Mbweni wakati alipokuwa akizungumza na vikundi vya usafishaji vya WAJAMAMA ambayo ni kampuni inayoweka akinamama na watoto katika hali ya usafi na kuwa na afya bora  wakishirikiana  na Safisha Zanzibar  kwa lengo la kuona mji unakuwa safi na unavutia .

Amesema jamii inaona labda usafi ni wa Serikali peke yake au Manispaa  dhana hiyo iondoshwe kwani kila binaadamu au kiumbe chochote kinahitaji kuwa na mazingira ya usafi sehemu anayoishi hivyo jitihada za kutoa elimu zinahitajika zaidi.

Hata hivyo, amesema iwapo usafi utakuwemo nchini maradhi ya mripuko hayataweza kutokea Bajeti ya dawa itapungua  uchumi utaongezeka    kwa sababu wananchi watakuwa na afya nzuri na hilo ndio  lengo la Serikali.

“Iwapo usafi utadumishwa jamii itaishi kwa kuwa na afya njema itaepukana na maradhi ya mripuko na ndio azma ya Serikali yetu”, alisema Waziri huyo.

Aidha amesema mji unapokuwa safi mazingira yanapendeza  hata watalii wataongezeka vijana watapata ajira na pato la Serikali litaongezeka.

Akielezea changamoto kwa jamii amesema bado haina uelewa wa kutia taka ndani ya sehemu maalum inayowekwa na manispaa na hili ndio linalosababisha kuzagaa kwa taka ndani ya mji.

Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii  Zanzibar Abdullah Mohamed Juma, amesema Nchi inategemea utalii kwani ndio uti wa mgongo hivyo tusafishe mji na kuweka mazingira yaliyo safi ili watalii waje kwa wingi.

Pia amesema taka ni rasilimali ambayo  inasarifiwa duniani na kwa hapa Zanzibar imeanza kukusanya chupa ambazo zishatumika kwa kusarifiwa na  nchi za wenzetu taka hufanyiwa baadhi ya mambo mengine kama vile mbolea na umeme.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Wilaya ya Magharibi ‘B’ Abdullah Saidi Natepe, ameitaka jamii iwache tabia ya kutupa taka ovyo kwani kufanya hivyo kunapelekea kuchafua mazingira.