NA HUSNA MOHAMMED

LICHA ya Serikali ya Mapinduzi kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, lakini baadhi ya watendaji wanarejesha nyuma juhudi hizo, jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo wawekezaji hasa wa sekta ya viwanda.

Hayo aliyasema jana Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali, katika hoteli ya Verde mjini hapa wakati akifungua mkutano wa wadau wa biashara kuhusiana na kuwashawishi wawekezaji katika maeneo maalumu ya viwanda yaliyotengwa na serikali.

Balozi Amina alisema kufanya kazi kwa mazoea unaochangiwa na urasimu kwa kiasi kikubwa unadhoofisha juhudi za serikali katika kuleta maendeleo ya dhati hasa sekta ya viwanda na biashara.

“Dunia hivi sasa imebadilika ni lazima kuacha kufanya kazi kwa mazoea, kufanya hivyo hatutapiga hatua ya maendeleo kwa baadhi ya watu wachache wenye urasimu, serikali baadhi ya maeneo tayari imeshaweka miundombinu rafiki ya wawekezaji kufika lakini urasimu huo unakwamisha wawekezaji wenye nia ya kuwekeza”, alisema. 

Akitolea mfano wa maeneo hayo ni pamoja na eneo la uwekezaji liliopo Dunga, Uwanja wa ndege Unguja na eneo la Chamanangwe Pemba.

“Nikiri kuwa baadhi ya maeneo kweli bado hatujaweka mazingira rafiki kama vile Dunga, eneo huru la Micheweni, lakini kama Chamanangwe tayari kuna barabara nzuri, umeme na huduma nyengine sambamba na eneo huru la Fumbalina kila sifa ya uwekezaji”, alisema.

Alisema baadhi ya nchi duniani kuna mfumo mmoja tu unaoshirikisha taratibu zote za uwekezaji lakini hapa wanapokuja wawekezaji wanahangaishwa jambo ambalo linawakatisha tamaa na kubakia kusamehe.

Hivyo aliwataka wahusika kuwa na maneno machache na vitendo kuwa vingi, ili kuona kwamba Zanzibar inapiga hatua katika uwekezaji.

Hata hivyo, Balozi Amina aliwataka Jumuiya ya wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo na kuwashawishi wawekezaji wa ndani nan je kuja Zanzibar.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara ZNCC, Tawfiq Salim Turky, alisema kwa kuwa serikali imeonesha njia basi fursa hii itatumika haraka na ndio sababu ya kufanyika kwa mkutano huo.