BEIRUT, LEBANON

WAZIRI Mkuu mteule wa Lebanon amejiuzulu wadhifa huo baada ya mwezi mmoja wa kujaribu bila mafanikio kuunda baraza la mawaziri lisiloegemea kundi lolote.

Mustapha Adib aliyewahi kuhudumu kama balozi wa Lebanon nchini Ujerumani,aliteuliwa na rais wa nchi hiyo kuwa waziri mkuu mwishoni mwa mwezi uliopita.

Serikali iliyopita ya Waziri Mkuu Hassan Diab ilijiuzulu baada ya kutokea mripuko mkubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut Agosti mwaka huu.

Adib aliwaambia waandishi wa habari anajiuzulu kwani imekuwa dhahiri kwamba aina ya baraza la mawaziri alilotaka kuliunda litashindwa.

Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa kutoafikiana na Waislamu wa Shiite juu ya uteuzi wa Waziri wa fedha ilikuwa moja ya kikwazo kikubwa.