NA FAT-HIYA MOHAMMED, WEMA
NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema Wizara ya Elimu itaendelea kutoa Elimu kupitia redio na television ili kukuza viwango vya ufaulu nchini.
Amesema hayo wakati alipokutana na wawakilishi kutoka ubalozi wa Korea Kusini huko ofisini kwake Mazizini, ambapo alisema kuwa wakati wa janga la maradhi ya corona hapa nchini skuli zilifungwa hivyo redio na televisheni ndizo zilizokuwa zikirusha vipindi vya masomo.
Alisema katika kipindi cha janga la maradhi hayo wizara ya Elimu ilichukua jitihada za kutoa elimu kupitia redio na televisheni kwa kipindi chote cha kufungwa skuli hali iliyowasaidia wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu kupata matokeo mazuri.
Naibu huyo alisema juhudi za kutoa elimu kwa njia hiyo zimesaidia kuongeza ufaulu wa daraja la kwanza na la pili kwa kidato cha sita, hivyo ipo haja ya kuendelea na utaratibu huo ambao umeonesha manufaa.
Kwa upande wake balozi wa Korea Kusini, Heashin alisema lengo la kufika wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ni kufuatilia maendeleo ya mradi wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa sekondari kupitia redio na televisheni katika kipindi chote cha ugonjwa wa corona.
Balozi huyo alisema katika mradi huo pia wameweka kipengele cha kujengewa uwezo walimu ambao watashiriki katika kuendesha vipindi vya masomo kupitia redio na televisheni.
Aidha balozi huyo aliipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kwa kuchukua juhudi kubwa za kupambana na maradhi ya corona na kufanikiwa nchi kuwa hali ya salama.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Utawala na Uendeshaji Mwalimu Abdullah Mzee Abdullah alisema wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ipo tayari kushirikiana na Korea Kusini.
Alisema kazi iliyopo hivi sasa wapo katika hatua za mwisho kupata masafa ya mawasiliano (frequency) ambayo yatasaidia kurusha vipindi vya masomo moja kwa moja.
Naibu huyo alisema vipindi hivyo vimeandaliwa katika studio zilizopo chini ya wizara yake na kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Kiasi cha dola 200,000 zilitolewa na ubalozi wa Korea Kusini kwa ajili ya kufadhili vipindi vya masomo kupitia redio na televisheni kwa kipindi chote cha maradhi ya corona na kuandaa masafa(frequency) kwa ajili ya kurusha vipindi hivyo kwenye masafa marefu.