NA MARYAM HASSAN

MKURUGENZI wa idara ya Maandalizi na Msingi katika wizara ya elimu na mafunzo ya amali (WEMA) Safia Ali Rijali, amewataka walimu wa madrasa kuwafundisha wanafunzi wao tafsiri ya Qur-ani ili wawe waadilifu.

Wito huo ameutoa wakati akifungua mafunzo ya walimu wa madrasa katika ukumbi wa skuli ya Kidutani wilaya ya Mjini, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema imebainika kuwa wanafunzi wengi wanahifadhishwa kur-an lakini hawajui maana ya maneno waliyoyahifadhi jambo ambalo linawafanya kwenda kinyume na mafunzo yaliyomo katika kitabu hicho.

Alisema iwapo watafanya hivyo, kutapelekea kupata jamii bora kutokana na mafunzo wanayoyatoa jambo ambalo litakuwa na tija zaidi.

“Endapo mtakuwa na utaratibu huu, watoto wetu watakuwa wanajua lipi jema na lipi baya kwa sababu makatazo na maelekezo ya namna watu wanatakiwa waishi yameelezwa katika kur-an,” alisema.

Aidha aliwataka walimu hao kubuni mbinu bora za kuwasimamia watoto ili waisome vyema elimu ya dini kwa amani na kuyafanyia kazi mafundisho yake.

Akizungumzia suala la udhalilishaji, mkurugenzi huyo aliwaomba walimu hao kudhibiti vitendo hivyo kwa kutojihusisha navyo lakini pia kuwafundisha wanafunzi wao athari zake katika maisha ya duniani na kesho akhera.

“Kumekuwa na malalamiko kuwa baadhi ya walimu wa madrasa wanajihusisha na vitendo vya udhalilishaji. Jambo hili halipendezi na linachafua haiba ya dini yetu na kuondosha uaminifu miongoni mwa jamii,” alisema.