NA SAIDA ISSA, DODOMA

WIZARA ya Fedha na Mipango imezindua mpango wa maendeleo ya sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 2019/2020 hadi 2029/2030, ambao umelenga kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi.

Akizindua mpango huo jijini hapa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dotto James, Naibu Katibu Mkuu Mary Maganga alisema mpango huo utaongeza wigo katika upatikanaji wa huduma za mikopo, akiba, uwekezaji na uongezaji mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na sekta ya viwanda.

Aidha, aliongeza kuwa mpango huo umeandaliwa ili utumike kama nyenzo ya kutatua changamoto zilizopo ambapo pamoja na mambo mengine pia umelenga kuongeza upatikanaji mitaji ya muda mrefu, upatikanaji huduma jumuishi za fedha na kulinda watumiaji wa huduma za fedha.

Alibainisha kuwa mpango huo wa miaka 10 unaolenga kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha, kudhibiti utakatishaji fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika sekta ya fedha.

Kwa upande wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti amewataka kutumia fursa zilizopo katika mpango huo na kujipanga katika kuboresha maeneo mbalimbali ya kitaaluma na kiutafiti ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuwa yenye ushindani na kuweza kuhimili mabadiliko ya nyakati kwa wepesi na weledi.

Akitoa maelezo ya mpango huo, Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Dk. Charles Mwamwaja alisema wakati wa maandalizi, timu ya wataalam wa mpango huo ilifanya mapitio kwenye nyaraka mbalimbali zikiwemo taarifa za maboresho ya sekta ya fedha.

Pia ilipitia mpango wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2016/17-2020/21 na taarifa ya programu ya tathmini ya sekta ya Fedha ya mwaka 2018 kwa lengo la kupata matokeo zaidi katika utekelezaji wa mpango mkuu wa kitaifa.