NA ASYA HASSAN

MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) imesema wapo baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Hayo yalisemwa na Ofisa Uhusiano wa taasisi hiyo, Yussuf Juma Silim alipokuwa akizungumza na watumishi wa Kampuni ya Maendeleo ya mafuta na gesi asilia, hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) uliopo Maisara, Zanzibar.

Alisema wapo baadhi ya viongozi na watumishi wanaendelea kuchukua rushwa licha ya kuwa serikali inakemea tabia hiyo hatua ambayo inachangia kudumaza na kuwafanya watumishi kushindwa kutekeleza majuku yao ipasavyo, hali ambayo inaongeza umaskini kwa wananchi. “Rushwa sio kupokea na kutoa kitu tu kama ilivyozoeleka lakini pia hata mtu kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa lengo la kujipatia maslahi binafsi pia rushwa jambo ambalo hurejesha nyuma maendeleo ya nchi,” alisema.