GITEGA,BURUNDI

KIKUNDI cha wakimbizi 511 wa Burundi wanarejeshwa nchini mwao kutoka Kambi ya Wakimbizi ya Mahama iliyoko Wilaya ya Kirehe, Mkoa wa Mashariki.

Kwa muibu wa Wizara ya Usimamizi wa Dharura (Minema), kikundi hicho kiliondoka kambini saa 6:20 asubuhi Alhamisi, Septemba 24, kuelekea Nemba Wilayani Bugesera, Mkoa wa Kusini.

Hili ni kundi la tatu kurudishwa nyumbani baada ya kuzuka kwa janga la Covid-19.

Takwimu za Wizara hiyo zinaonyesha kuwa kundi la kwanza la wakimbizi wa Burundi waliorejeshwa lilikuwa na 485, wakati la pili lilikuwa na jumla ya wakimbizi 507 wa Burundi.

Wizara hiyo pia inasema kwamba kundi jengine la wakimbizi wa Burundi wa mjini linatarajiwa kurudishwa Alhamisi wiki ijayo.

Kabla ya Rwanda kufunga mipaka yake kwa kuzuia Covid-19, kati ya 2015 hadi Machi 2020, wakimbizi 5,222 walikuwa tayari wamerudi Burundi kwa hiari.