NA HAFSA GOLO

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imekubaliana na pingamizi za wagombea 15 wanaowania ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani saba kutokana na kutofuata sheria na kanuni za uteuzi wa Tume hiyo.

Mkurugenzi wa Tume hiyo, Thabit Idarous Faina, alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitoa taarifa ya maamuzi ya pingamizi kwa wagombea.

Mkurugenzi huyo alisema Tume ilipokea jumla ya pingamizi 125, kati ya hizo pingamizi 84 kwa upande wa uwakilishi na 41 kwa udiwani kutoka wilaya 11.

Alisema baada kuzipitia pingamizi hizo, Tume imebaini kuwa wagombea 15 wa nafasi za uwakilishi na saba kwa upande wa udiwani walishindwa kufuata sheria na kanuni za uteuzi wa Tume hiyo.

Aliwataja wagombea walioenguliwa nafasi ya uwakilishi kutoka Chama cha ACT- Wazalendo ni Haji Ali Haji (Tumbatu), Hassan Jani Masoud (Nungwi), Haji Mwadini Makame (Kijini) na Juma Duni Haji (Mtoni).

Wengine ni Hasne Abdalla Abeid (Bububu), Hamad Masoud Hamad (Ole), Omar Ali Shehe (Chake Chake), Khamis Rashid Khamis (Chonga), Issa Said Juma (Konde), Mmanga Mohamed Hamid (Tumbe) na Ishaq Ismail Sharif (Wete).

Aliwataja wengine ni Othman Ali Khamis wa Chama cha Mapinduzi (Mtambwe), Juma Ali Juma CUF (Ole), Abass Omar Abass Chama cha Makini (Ole) na  Yussuf Said Hamad  Chama cha UPDP (Chake Chake). 

Akifafanua zaidi alieleza kwamba rufaa hizo zilizowasilishwa ZEC kutoka ngazi ya wilaya ziligawika katika makundi ya aina saba kulingana na aina ya kasoro iliyowekewa pingamizi.

Akitoa ufafanuzi kuhusu makundi hayo alisema, kundi la kwanza linahusu pingamizi kwa wagombea walioandika umri kimakosa katika fomu zao za uteuzi.

Hata hivyo alisema Tume imezikataa pingamizi hizo kutokana na kuwa kasoro hizo ni za kibinaadamu zinazoonesha mgombea hakuwa na nia ya kudanganya.

Akizungumzia kuhusu kundi la pili alisema, kundi hilo linahusu pingamizi na rufaa kwa wagombea walioandika taarifa za makaazi kimakosa katika fomu za uteuzi lakini kutokana na hawakukusudia kuidanganya Tume imewaachia.

Alisema kundi la tatu ambalo linahusu pingamizi kwa wagombea lilikuwa ni la watumishi wa umma ambao walikosa ruhusa kwa waajiri wao suala ambalo ni kinyume na kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Utumishi wa umma namba 3 ya mwaka 2003.

Kuhusu wagombea waliodhaminiwa na wanachama ambao wamemdhamini zaidi ya mgombea mmoja katika uchaguzi mmoja ikiwa ni kinyume na kanuni ya 15 (2) ya sheria ya uchaguzi ya Zanzibar ambayo inaelekeza kuwa kila mdhamini ataruhusiwa kumdhamini mgombea mmoja kwa kila uchaguzi.

Kwa upande wa kundi la wagombea walioghushi vyeti vya kuzaliwa alisema, ZEC imewaengua wagombea hao kutokana na kushindwa kuwasilisha vielelezo vyao ambavyo vinathibitisha uhalali wa nyaraka.

Alisema kundi la sita lilikuwa ni rufaa za wagombea walioshitakiwa kwa kosa la jinai na kushindwa kubainisha makosa katika fomu zao hivyo ZEC imewaengua wagombea hao.

Aidha alisema, kundi la saba lilikuwa kwa wagombea walioshindwa kufuata kanuni za uchaguzi katika kujaza fomu za uteuzi ,kutokana na ukakasi wa kasoro hizo za ujazaji wa fomu za uteuzi, wagombea hao ZEC imewaengua.