NA LAILA KEIS

MKUU wa kitengo cha huduma za sheria katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khamis Issa Khamis amesema Tume hiyo haitasita kuwachukulia hatua wanasiasa na wananchi wenye kutumia vibaya mitandao ya kijamii kuchapisha taarifa za kisiasa zenye viashiria vya uvunjifu wa amani.

Mkuu huyo alieleza hayo jana huko ofisini kwake Maisara mjini Zanzibar alipozungumza na Zanzibarleo.

Khamis alisema kumejitokeza baadhi ya watu kutumiwa na wanasiasa kurusha taarifa za kisiasa ambazo zina viashiria vya uvunjifu wa amani, uchochezi na kuhatarisha umoja miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema kufanya hivyo ni kosa na kwamba Tume haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wenye kurusha taarifa hizo ambazo hazilengi kudumisha umoja miongoni mwa wananchi.

“Kumejitokeza baadhi ya wamiliki wa mitando ya kijamii kutumiwa na wanasiasa katika kipindi hichi cha kampeni na uchaguzi mkuu kwa kurusha taarifa zenye viashiria vya uchochezi miongoni mwa wananchi”, alisema.

Hivyo, aliwataka wananchi na wanasiasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu, wasitumie mitandao kama njia ya kutupa vijembe na kusema uongo ambao utapelekea uvunjifu wa amani katika nchi yetu.

Aidha alisema, vyama vyote vya siasa kwa kushirikiana na serikali, wameamua kufanya uchaguzi kwa amani, hivyo aliwataka na wananchi na mashabiki wa kisiasa nao kuhakikisha amani inadumishwa.

Alisema kama ilivyo katika sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, kanuni za uchaguzi mwaka 2020, kuwa kiongozi wa chama cha siasa, mwanachama, mshabiki au mtu mwengine yeyote ajiepushe na vitendo vyovyote vinavyopelekea kuibua hisia za chuki, vitisho au fujo.

Aidha mkuu huyo alisema, serikali kupitia vyombo husika, hawatowaacha wale wote ambao watabainika kuandika au kusambaza ujumbe wowote wa uchochezi.

“Nawasihi wanasiasa wavitumie vizuri vyombo vya habari vikiwemo vya kijamii ili kufikisha ujumbe wa ilani na sera zao, na sio kuvitumia vyombo hivyo kupandikiza chuki na uhasama miongoni mwa wananchi wa Zanzibar”, alisema.