NA ABOUD MAHMOUD
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) limeshauriwa kuanzisha ligi kuu kanda ya Unguja na Pemba, ili kupatikana ufanisi wa mchezo huo baada ya timu zote za Pemba kushuka daraja.
Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu kocha mkuu wa klabu ya Chipukizi yenye maskani yake Chake chake Pemba, Mzee Ali Abdallah alisema kufanya hivyo kutasaidia kuinua viwango vya wachezaji.
Alisema ni vyema kucheza ligi ya kanda na baadae kupatikana washindi ambao watacheza ligi kuu ya Zanzibar kwa kushirikisha timu za Pemba na Unguja.
“Ushauri wangu kwa ZFF kuanzisha ligi ya kuu Unguja yao na Pemba yao, hii itasaidia kupatikana timu nane, nne kutoka kila upande na baadaye kusaka bingwa wa Zanzibar,”alisema.
Alisema kuendesha michezo ni gharama na klabu takriban zote havina uwezo, hivyo ni vizuri kubuni mpango huo ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Kuhusu klabu yake ya Chipukizi ambayo imeshuka daraja, kocha huyo alisema mpaka hivi sasa, wanasubiri maamuzi kutoka kwa ZFF, kwani klabu zote za Pemba zilizokuwa zikicheza ligi kuu zimeshuka daraja na ligi ya kanda bado inaendelea.
Alifahamisha kwamba maamuzi yatakayotolewa na ZFF yatakua sahihi kwao, ikiwa kutakiwa kucheza ligi kuu au kanda na kusema kwamba, klabu yao imedumu kwa miaka mingi kwenye ligi kuu.
“Maamuzi yatakayotolewa na ZFF tutayafuata, kama kucheza ligi kuu au kucheza kanda, najivunia klabu yangu imecheza muda mrefu ligi kuu, na imewahi kushuka daraja kwa hiyo sio jambo la ajabu kwetu,”alisema Mzee.